You are here
Habari 

Kamati ya gesi, mafuta Tanzania Bara, Zanzibar kuundwa

Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Mhandisi Kapuulya Msomba (katikati) akisisitiza jambo katika kikao hicho.

Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na  Wizara ya  Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Zanzibar zinatarajia kuunda Kamati Maalum kwa ajili ya  kuandaa Mpango wa ushirikiano kati ya Tanzania Bara na  Zanzibar katika  sekta za gesi na mafuta.

Hayo yalielezwa mwishoni mwa wiki na  Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo  katika kikao chake na  Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Zanzibar, Salama Aboud Talib  aliyeambatana na Ujumbe wake.

Wengine waliohudhuria kikao  hicho ni  watendaji kutoka  Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo ya Petroli  Tanzania (TPDC),  Shirika la  Umeme Tanzania (TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti  wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Wakala wa Uagizaji  wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu wa Mafuta (PURA).

Profesa Muhongo alisema lengo la kamati hiyo ni  kujadili maeneo ya kushirikiana pamoja na kubadilishana uzoefu katika sekta  za gesi na mafuta

Alisema kuwa, kamati hiyo itashirikisha Wataalam kutoka katika  taasisi za Sheria, Ardhi, Kodi, Gesi na Mafuta  chini ya Makatibu Wakuu wa sekta husika kutoka Tanzania Bara na  Zanzibar.

Waziri Muhongo alisema kuwa, uwepo wa kamati hiyo utachochea Zanzibar kuwa na  taasisi kama TPDC na nyingine hivyo kupelekea ukuaji wa sekta ya gesi na mafuta.

Alisisitiza kuwa, Serikali ya  Tanzania Bara kupitia  Wizara ya Nishati na Madini ipo tayari kushirikiana na  Serikali ya  Zanzibar pamoja na kubadilishana uzoefu katika  masuala ya gesi na mafuta.

Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Mhandisi Kapuulya Msomba (wa tano kushoto, waliokaa mbele) akielezea majukumu ya shirika hilo katika kikao cha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Zanzibar, Salama Aboud Talib aliyeambatana pamoja na ujumbe.

Profesa Muhongo alishauri  Serikali ya  Zanzibar kuandaa wataalam wa mafuta  na gesi  kwa kuwasomesha katika ngazi za diploma na shahada katika Chuo Kikuu cha  Dar es Salaam (UDSM) na  Chuo cha Madini  Dodoma (MRI).

Akiongeza kuwa, Serikali ipo tayari kutoa ufadhili  kwa wanafunzi wa Zanzibar wanaofanya vizuri katika masomo ya  Sayansi kwa ajili ya kusomea shahada ya uzamili katika  vyuo vya  ndani na nje ya nchi.

 Naye Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Zanzibar, Salama Aboud Talib, alimshukuru Waziri Muhongo kwa utayari wa Wizara  ya Nishati na Madini  katika kushirikiana na Wizara yake kwenye shughuli za mafuta na gesi

Alisema kuwa,  kamati itakayoundwa itapelekea mambo kwenda kwa kasi na kuwa na data za pamoja zinazotokana na utafiti wa mafuta na gesi na kupanga Mikakati  ya kuvutia wawekezaji kutoka nje ya nchi.

Mwandishi: Mwandishi Wetu kutoka Raia Mwema
Tembelea Chanzo

Related posts