You are here
Michezo Kimataifa Slideshow 

KIVUMBI LIGI YA MABINGWA ULAYA LEO

LONDON, ENGLAND

UHONDO wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, unatarajia kuendelea leo kwenye viwanja mbalimbali, huku kwenye Uwanja wa Wembley, Tottenham wakiwakaribisha wapinzani wao ambao ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo Real Madrid.

Oktoba 17, mwaka huu timu hizo mbili zilikutana kwenye michuano hiyo, huku Madrid wakiwa kwenye Uwanja wa nyumbani wa Santiago Bernabeu walilazimishwa sare ya bao 1-1, hivyo leo hii kila timu inataka kuonesha uwezo wake ili kuibuka na ushindi ili kujitengenezea nafasi.

Tottenham wameweka wazi kuwa wapo tayari kumtumia mchezaji wao, Harry Kane, katika mchezo huo wa leo baada ya kusumbuliwa na tatizo la nyama za paja. Mchezaji huyo amekuwa nje ya uwanja wiki sasa baada ya kuumia katika ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Liverpool.

Tangu mchezaji huyo awe nje ya uwanja, amekosa michezo miwili na michezo yote Tottenham imekuwa ikipoteza kama vile dhidi ya West Ham kwenye Kombe la Ligi pamoja na Manchester United mwishoni mwa wiki iliyopita. Kutokana na hali hiyo, Tottenham wanaamua kutaka kumtumia mchezaji huyo leo hii.

Katika michezo mitano ambayo Tottenham wamecheza hivi karibuni, imefanikiwa kushinda miwili, kutoa sare mmoja na kufungwa miwili, wakati huo Real Madrid ikishinda mitatu, kufungwa mmoja na kutoa sare mmoja.

Timu hizo mbili katika michezo minne waliokutana, Tottenham haijawahi kufanikiwa kushinda, lakini Real Madrid imeweza kushinda mara tatu na sare moja.

Michezo mingine ambayo itapigwa leo hii ni pamoja na Napoli ambao watakuwa kwenye uwanja wa nyumbani na kuwakaribisha wapinzani wao vinara wa Ligi nchini England, Man City.

Oktoba 17, Napoli walikubali kichapo cha mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Etihad katika michuano hiyo na leo wanataka kulipa kisasi wakiwa nyumbani. Katika michezo mitano waliocheza Napoli hivi karibuni wamefanikiwa kushinda mitatu na kufungwa mmoja dhidi ya Man City na sare mmoja, wakati huo Man City wakishinda michezo yote mitano.

Timu zingine za leo ni Besiktas dhidi ya AS Monaco, Borrusia Dortmund dhidi ya Apoel Nicosia, FC Porto dhidi ya RB Leipzig, Liverpool wakicheza dhidi ya NK Maribor, Sevilla wakicheza na Spartak Moscow, Shakhtar Donetsk dhidi ya Feyenoord.

Mwandishi: Mtanzania Digital kutoka Mtanzania

Related posts